Home » Fanuel Mlenge, Lifestyle

Starehe Gharama

Na FANUEL MLENGE
Published August 3, 2009

Siku hiyo niliwahi kutoka skuli. Tumbo liliniletea `matataizo,’ hali ambayo ilihatarisha hali ya upendo, umoja na mshikamano uliojengwa kwa karne nyingi kule tumboni. Sikuwa na jinsi zaidi ya kujitoma kwenye daladala kuwahi nyumbani. Si wajua vile maskuli yetu hayana kasma ya kumtibisha mwanafunzi?

Kufika tu kituoni, daladala hilo! tena tupu, “limepigwa mswaki” na menziye yaliyozidi kete. Ile naingia tu, konda akanidaka.

“We wa-kusoma! Unakaa kwenye kiti kwani utalipa nauli ya mtu mzima?” Akanizuia kuketi, japo gari liliondoka likiwa bado vile vile `swaki.’

Baada ya kusimama kwa muda, nilihisi hali kuzidi kuwa mbaya, na “breki” niliyodhibitia vilivyomo tumboni ilikaribia kufeli. Na kufeli kwa breki hiyo kungefanya vilivyomo tumboni vitoke kwa kasi isiyo na kidhibiti-mwendo. Na kwa kuwa nilikuwa nimesimama peke yangu kwenye gari tupu, nilionekana na kila abiria. Hivyo basi kitendo cha kufanya `majambozz’ mle mle ndani ya gari kungenigeuza kideo cha bure!

Nikambembeleza kondakta aelewe matatizo yalonikumba mwana wa mwenzie, lakini hakuelewa somo.

“Jaribu kuvuta subira. Maombi yako yamepokelewa, na kimsingi yanafanyiwa kazi. Uwe mstahimilivu wakati ngazi zinazohusika zinashughulikia suala lako,” alisema.

Kwa upande wangu ningeweza kuvumilia, lakini tatizo lilikuwa lile tumbo halikupenda kuelewa mazingira magumu yaliyonikabili.

Nikapiga moyo konde. “N’talipa nauli ya mtu mzima ili niketi, nisiadhirike.”

Taratibu nikajikongoja mpaka kwenye siti `poa’ ya dirishani, na kuketi kwa madaha.

“Utalipa nauli kubwa?” alitaharuki konda.

“Ndiyo n’talipa.”

“Aah! Lete kabisa!” Akajitwalia `haki’ yake.

Baada ya kuketi, nilihisi ka-nafuu fulani kwenye `breki’ ya tumbo, kwani kiti nacho kilisaidia kupunguza makali ya vitu vilivyokosa subira kule tumboni. Lo! Kuketi ni raha. Kumbe starehe gharama!

Kituo kilichofuata kondakta alicheka mpaka gego la mwisho alipolifuma `nyomi’ kundi kubwa la abiria waliolizonga gari lake.

Na kweli. Walipoingia wote, gari likawa “bomba,” abiria wakashonana kana kwamba waliambiwa gari ile nd’o ya mwisho.

Kando yangu alisimama mzee wa makamo. Mzee yule alikuwa anakikodolea macho kiti nilichokalia akitegemea n’tampisha.

Sikumpisha.

Kwa kuwa siti “inanunuliwa” kwa `nauli kubwa,’ sikuona sababu ya kumpisha. Ukiongeza na hali ya `machafuko’ tumboni, nafasi ya yule mzee kupishwa na miye ikazidi kuwa finyu.

Akaanza abiria mmoja `mpambe.’

“Hivi huyo mtoto hana adabu?” Hamwoni mtu mzima amesimama wakati yeye ameketi?”

Kundi kubwa la abiria likasapoti, hasa wale waliokuwa wamesimama jirani na mimi. Bila shaka walikuwa wakitegemea watajipatia ahueni ya kusongamana.

Kondakta akaja mbio kutaka kunitoa.

“We `denti! Wapishe wenzio wanaolipa nauli kubwa!” alisema kwa ukali.

Sikutaka ubishi. N’kamtolea tiketi `kubwa’ aliyonipa mida michache iliyopita.

Akanywea.

Nikaendelea `kula nchi’ kwenye siti ile; sikutaka `kuangalia makunyanzi.’

Akasogea mama mjamzito. Pengine walitegemea n’tamuonea `imani.’ Lakini kwa kuwa sikuwa ni abiria pekee mwenye kulipa nauli kubwa, nilijikausha, nikingojea `wasamaria wema’ wampishe. Hakujitokeza `msamaria’ yeyote. Wote macho yao yalikuwa kwangu.

“Yaani we mwanafunzi hata huyo mama yako huwezi kumpisha?” alisema baba mmoja aliyeketi siti jirani.

Kama kawaida niliamua `kuuchuna’ kimya. Na yule mama sikumpisha. Akawa ananikodolea macho.

Abiria wengine wakaungana kunitupia `madongo.’ Wakati wanaendelea na makombora yao, alijitokeza `fyatu’ mmoja aliyeamua kunitetea.

“Mwacheni kijana ale matunda ya jasho lake!” alisema na kufanya wengine wasonye na kumshutumu. Yeye hakujali, akaendelea `kuwapasha.’

“Yule kijana alipoambiwa asimame ilhali viti vipo wazi hakuwepo hata mmoja aliyeibuka kumtetea. Hivi sasa anakula matunda ya jasho lake mnaanza kumletea mizengwe! Acheni naye ale starehe. Starehe gharama! Zimemtoka pesa kuipata siti hiyo …”

Nilishuka kwenye basi niwahi kwnda kujisetiri. Huko nyuma nimeacha mjadala mkali. Sifahamu uliishaje, lakini siku hizi nimenogewa. Ninapoenda shuleni hulipa nauli `kubwa’ na kupata starehe ya kuketi kwenye siti. Wakati na starehe, watu mbalimbali huwa `vishingo’ wakitegemea n’tawapisha. Lakini konda akishachukua nauli `kubwa’ hajali tena zaidi.

Raha iliyoje!


Reach Fanuel Mlenge at editor@eafricainfocus.com

________________________________________
Copyright © 2009 Mlenge Fanuel



Related Posts

Ng’ombe wa Maskini, Mama Mwajey, Nihame bondeni! nimelongwa?

Author Profile: editor Story  on August 2, 2009, No Comment
Digg this!Add to del.icio.us!Stumble this!Add to Techorati!Share on Facebook!Seed Newsvine!Reddit!

Trackbacks/Pingbacks

  1. Starehe Gharama - Mashada Forums

Leave a Reply:

You must be logged in to post a comment.


Home of Hope

  Copyright ©2009 East Africa in Focus, All rights reserved.| Website developed by: personalized-websites.com.                                             Staff Login