Ng’ombe wa Maskini
Na FANUEL MLENGE
Published July 19, 2009
Mzee Pantike alikuwa ni maskini. Au pengine ndivyo alivyofikiri, na kusema kila mara.
“Sisi watu maskini tuna taabu sana! Maisha yetu ni dhiki tupu!”
Hali ya mzee Pantike ilikuwa ya malalamiko kila siku.
“Wanangu siwezi kuwanunulia nguo za sikukuu kwa vile mimi ni maskini!” Na alikuwa na watoto wengi.
Jambo hili lilikuwa gumu kueleweka kwa watoto wa mzee Pantike.
“Mbona watoto wenzetu wana hali bora kuliko sisi?” waliuliza. Hasa Numbelya ndiye aliyekuwa mdadisi sana.
“Baba, kama wewe ni maskini, mbona una ng’ombe wengi sana?” Aliuliza kila siku.
Na kila mara alipouliza swali hilo, baba yake alikuwa mkali.
“Ng’ombe hawa si wako zizini? Kwani hao wanaweza kuleta nguo?”Alifoka.
“Lakini baba, si tungevuna ng’ombe kidogo kila mwaka? Na sisi tungevaa vizuri kama akina Doto. Tungefanya sherehe siku ya Krismasi kama watoto wenzetu. Na tena tungeweza hata kusoma shule bora zaidi!” Alijibu Numbelya
Wakati huo wadogo wake Numbelya walikaa kimya. Walijua jinsi baba yao anavyowapenda ng’ombe wake. Hujihisi raha isiyo kifani anapowaona.
Hakuna mtu aliyejua idadi kamili ya ng’ombe wa Mzee Pantike. Wengine walisema anao ng’ombe elfu moja, Wengine walisema elfu kumi. Na wengine kusema laki moja. Ilisemekana majirani yake walikuwa wanaiba ng’ombe wake mmojammoja bila Mzee Pantike kujali. Ndiyo maana majirani hao waliweza kuuza maziwa, ngozi na nyama zaidi ya Mzee Pantike mwenyewe, japo wao hawakuwa na zizi hata moja.
Akiulizwa anao ng’ombe wang’api Mzee Pantike hucheka tu. Mbuzi, kondoo, kuku na bata hao ndio kabisa hawakuwa na idadi! Kila awaonapo ng’ombe wake wakifika na kurudi Mzee Pantike alisahau maneno yake ya siku zote:
“Sisi watu maskini tuna taabu sana! maisha yetu ni dhiki tupu!”
Hutabasamu na kucheka na wanawe. Hasa Numbelya anapokuwa hakurudi kutoka kucheza. Maswali ya Numbelya siku zote yalimfanya mzee Pantike akose raha.
“Baba, mbona Mzee Pangalamawe anao ng’ombe wachache kuliko hawa. Lakini si unaona akina Doto, Nungumaji na wenziwe wanavyopendeza? Wanapata nguo mpya kila mara. Wakati wa sikukuu ndio usiseme! Nyumba yao ya matofali, ina bati na umeme….”
Hali hii iliendelea kwa muda mrefu. Lakini siku zote Mzee Pantike alijitetea kwamba yeye ni maskini na kwamba siku Numbelya na nduguze wakikua, watawatumia ng’ombe wapendavyo! mradi tu wajiletee utajiri.
Siku hizi zote Numbelya alikuwa akilalamika.
“Hii nyumba haiwezi kuwa na maendeleo, mpaka huyu mzee na mawazo yake ya kimaskini yatakapobadilika!”
Siku moja mzee Pantike aliwaita wanawe wote,
“Wanangu mimi nishakuwa mzee. Mambo ya kuhangaika na ng’ombe siyawezi tena,naenda zangu kwenye kibanda changu cha shambani nikapumzike. Siku nyingi nimekaaa huku. Hivi nawaachia ng’ombe wote, Kondoo wote, mbuzi wote, kuku na bata wote. Waangalieni na kuhakikisha wanaendela kuwepo. Mimi niliachiwa kiasi na babu yenu. Hakikisheni na ninyi mtakuwa na ng’ombe wa kuwachia wajukuu zangu!”
Ubishi ulizuka mara hiyo hiyo. Nani ndiye atakuwa ‘Mzee Pantike’ mpya! Nani awe ndiye mkubwa wa wenzake!
“mimi ndiye nafaa” Kila mmoja alisema.
Ilibidi Mzee Pantike aingilie kati. “basi jamani pigeni kura kuchagua mkubwa wenu!”
Wote walikubali wakapiga kura. Mzee Pantike akamtangaza mshindi
“Pakavu !!”
“Aaah! mbona ……” Numbelya na wenziwe wakapiga kelele.
Baba yao akasema wakikataa matokeo hayo atawanyima radhi.
“Mimi ndiye baba yenu. Matokeo niyasemayo ndiyo ya mwisho!”
Numbelya na wenzake wakakubali shingo upande Pakavu akawa mkubwa wa kaya. Ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na bata wakawa chini ya milki yake.
“Sasa basi Pakavu itisha mkutano wa kaya ili tujadili mbinu za kuondoa umaskini huu!” alisema Numbelya, na kuungwa mkono na wenziwe.
Pakavu akacheka kwa kebehi.
“Hivi si ninyi wenyewe mlinichagua?!” alisema
“ Hamna !” Alijibu Numbelya. “baba alikupendelea!”
Likawa zogo.
“Sasa tutajua nani ndiye mkubwa kwenye nyumba hii!” alisema Pakavu. “siitishi kikao cha familia! Na wala huyo Numbelya hawezi kufanya kitu chochote!”
Na kweli. Pakavu akaanza kufanya maamuzi ya peke yake.
“Si mlinichagua wenyewe!?” Alisema.
Kwanza alimwita rafiki yake Bangosho. Huyu Bangosho alikuwa tajiri. Japo hakuwa na ng’ombe wengi kama wao, alikuwa na nguo nzuri. Akampa kazi. Kazi yake ni kumfanya Pakavu na nduguze wawe matajiri sawa na Bangosho.
“Unafikiri hiyo itasaidia? Hawezi kukubali hata siku moja akufanye uwe tajiri kama yeye!” Alipinga Numbelya. “Amekuja kutunyonya tu!” alisema.
Pakavu alicheka
“Huyu Numbelya tunamjua alivyo mbishi. Kila jambo, hata la maana, yeye hupinga tu!” Alisema Pakavu. “Subiri na wewe zamu yako tuone utafanya nini!”
Maneno hayo hayakuwafurahisha nduguze. Wengi walimuunga mkono Numbelya.
“Hapana Pakavu! kwa nini umwite Bangosho aje wakati na sisi tunaweza kuchinja ng’ombe, kukamua ng’ombe maziwa, tunaweza kukata sufu za kondoo, tunaweza kuuza kuku na bata wenyewe?”
Pakavu hakukubali maneno yao.
“Jamani! “alisema. Si mnaona wenyewe sisi hatuna visu vikali kama vya Bangosho? Kwani nyie shida yenu nini? si mnataka na sisi tuwe kama Bangosho?”
Pakavu akampa Bangosho ng’ombe wote amwangalizie.
“Nitakufanya uwe tajiri kuliko mimi!” aliahidi Bangosho,
Kisha akalivamia zizi la Mzee Pantike kwa visu vikali. Ng’ombe dazeni kadhaa walichinjwa kila siku. Kilo na kilo za minofu zilipatikana .
Na Bangosho alizichukua na kupeleka kwenye mabucha yake.
“Sasa Pakavu! Kwa nini na sisi tusingeanzisha mabucha yetu ili nyama hii tuiuze wenyewe!?” Alipinga Numbelya.
Kama kawaida, Pakavu alicheka.
“Sisi tulivyo hivi maskini! Visu vyenyewe hatuna! Vile ovyo tulivyonavyo ni butu! Leo tunafikiria mabucha? Hebu mawazo yetu yaishie kwenye kutafuta tupa ya kunolea visu hivi. Au tukae kimya kungojea Bangosho aendelee kutuchinjia ng’ombe wetu.” Alisema.
Bangosho akazidisha kasi ya kuchinja na kuchuna ng’ombe. Akaleta visu vingi zaidi na zaidi. Tena vikali kuliko vile vya mwanzo. Punda wa Bangosho waliondoka usiku na mchana. Tena hakuna aliyejua ni nyama kilo ngapi wamebeba, Au maziwa lita ngapi.
Kama kawaida Numbelya hakukubali.
“Hivi wewe Pakavu, umeingia makubaliano gani na Bangosho?” Aliuliza.
“Si mlinichagua wenyewe!” akajibu. “Tumekubaliana kwamba kwenye kila ng’ombe atakayechinjwa,sisi tutachukua kipande cha mkia na nusu nundu!”
Familia nzima ikazomea. “Haaa! Haaa! Ah! Haiwezekani!!”
Pakavu akacheka. “Ninyi hamjui toka Bangosho amekuja, sisi ndio watoa nyama wakubwa hapa kijijini! Tena twazalisha nyama kwa viwango vikubwa kuliko vya Bangosho mwenyewe!”
Numbelya akainua chungu, na kummwagia maji ya ukoko.
“Yaani sisi tunapata vimkia tu! Halafu we wasifia hayo makilo ya nyama? Sisi yanatusaidia nini?”
Pakavu hakujali yale maji ya ukoko, wala maneno ya Numbelya.
Pakavu akatoa jedwali. Kwenye lile jedwali palikuwa na tarakimu nyingi, ambazo wenzake hawakuzielewa.
“Si mnaona! urari tulioanza nao, na huu tulionao hapa!” Alisema, meno yote nje kwa furaha, japokuwa wenziwe hawakumuelewa huo urari ni kitu gani.
Mara akaingia Nuru. Nguo zake viraka vitupu. Amekonda kwa utapiamlo.
“Nimerudishwa nyumbani sijalipa ada ya shule na mchango wa ….” Alisema.
“ Si mnaona!?” Aliingilia Numbelya. “Toka kuanza kuchinja hao ng’ombe, tumepata faida gani?”
“KELELE !!” Akafoka Pakavu. “mimi ndiye mkubwa nyumbani humu! Si mlinichagua wenyewe? Hivi mnafikiri utajiri utakuja siku moja kwa vile tu tunachinja ng’ombe?”
“Lakini kaka mbona wenzetu wenye ng’ombe…” alisema Nuru.
“KELELE!!” Akafoka tena Pakavu.
Nuru akanyamaza kimya.
Mara mvua kubwa ikaanza kunyesha. Kile kibanda cha manyasi kikavuja kama vile wako nje. Kila mtu akakimbilia sehemu ya kujibanza.
“Si unaona! Hata kubadilisha haya manyasi umeshindwa, wakati ng’ombe na Bangosho…” aliendelea kulalamika Numbelya.
“Hivi mnafikiri Bangosho atawatatulia matitizo yenu kila mtu? Kila mara ‘Bangosho! Bangosho! Bangosho! Bangosho! Bangosho! Bangosho! Mmezidi uvivu na wivu….!” Alijibu Pakavu.
Radi ilinguruma kwa nguvu. Kila mtu akajificha kichwa chake.
Walipoinua vichwa na kufungua macho, Pakavu ametoka. Yulee! Anaelekea machinjioni.
“Karibu!” Bangosho alimpokea kwa furaha.
Kisha akamtembeza machinjioni.
Lo! Kulikuwa kumebadilika! Ng’ombe sasa walikuwa wanachinjwa na mashine !
“Chukua hiki kizawadi chako Mzee!” alisema Bangosho, akimpa Pakavu chungu kilichojaa maini ya kuoka.
Mate yalimtoka Pakavu. Meno yake nje kwa furaha.
“Haya ndiyo matunda ya kumkaribisha Bangosho”
Aliporudi nyumbani alibeba makaratasi mengi zaidi. Yote yakionyesha majedwali yenye rangi za kupendeza zaidi. Yapendeza kuliko yale ya mwanzo!
“Haya we Numbelya! Hebu onja mafanikio yaliyotoka kwa Bangosho!!”
Numbelya hakusema kitu.Tayari amesikia minong’ono kwamba Bangosho hawapi hata hivyo vimikia na vipande vya nundu alivyokubaliana na Pakavu. Hutoa tu siku aliyojisikia, kwa maelezo kwamba siyo ng’ombe wote wenye nundu au mkia!
“Una habari Pakavu kwamba bado Nuru hawezi kwenda shule?” aliuliza Numbelya .
Pakavu akacheka, huku akikunjua jedwali lingine.
“Ifikapo mwakani sisi ndio tutakuwa wazalishaji nyama wakubwa kuliko wote kwenye historia! Haijapata kutokea wazalishaji nyama wakubwa kama sisi!”
Zogo kubwa likafumuka .
Habari ya mazogo ya nyumbani kwa mzee Pantike zilimfikia Bangosho. Akaona hatari ya kufukuzwa licha ya maini makavu anayompa Pakavu.
Sasa alianza kuchukua ng’ombe wazimawazima na kwenda kuchunia kijijini kwao!.
Alikuwa akiwachinja tu, na kupakia kila kitu kwenye mikokoteni, na kuwapeleka kwao .
Haikujulikana ni mikokoteni mingapi iliyo beba Ming’ombe ile usiku na mchana . Lakini Bangosho aliendelea kuhamisha Ng’ombe, na kwenda kuwachuna kwao “kabla familia ya mzee Pantike kuzinduka!”
Utajiri wa Bangosho sasa haukuwa na mfano! Na hapo hukusimuliwa hadithi ya mbuzi ,kondoo, kuku na bata.
Numbelya aliendelea kukerwa na ayaonayo. Aliendelea kupiga kelele kila siku, mpaka siku ile alipopotelea mitunduruni. Siku hiyo alichoka pale aliposikia kwamba binamuze Bangosho ndio watakuwa wanawapikia uji, kwa malipo ya vindama! Inasemekana Numbelya aliliwa na simba alipokwenda machungani. Wengine wanateta kwamba wale walikuwa ni “simba-watu “ waliotumwa na Bangosho au na Pakavu au na wote wawili.
Haikueleweka wajukuu wa Mzee Pantike walirithi nini, maana hata kwato na pembe zilizokuwa zibaki machinjoni , sasa hazikuwepo.
Nduguze Pakavu walibaki ndio watu maskini, fukara, na hohehahe pale kijijini kuliko hata ilivyokuwa mwanzo.
Copyright © 2009 Mlenge Fanuel










NYAKACH KILLINGS!
BETHANY CHILDREN'S HOME TANZANIA





Haya ni ya firauni. Yule bwana pakavu kaleweshwa na “ukubwa” wa “kujaguliwa” hata asiweze kujielewa mwenyewe.