Nihame bondeni! nimelongwa?
By: FANUEL MLENGE
Published July 1, 2009
HATA mimi nilikuwa nawashangaa wanaoishi mabondeni. “Kwa nini hawahami? Wanaona mchezo kuhama na kuhamia kila mwaka?” niliwaza.
Kila mkazi wa mabondeni niliyemuuliza kulikoni mambo haya! aliniona miye juha.
“Kwa nini?” sikuelewa.
Lakini hiyo ilikuwa enzi zile naishi kwenye nyumba ya shirika. Japo nyumba yenyewe haikuwa uzunguni halisi, ilikuwa kwenye `kota’ ambako hungeweza kupaita `uswahilini.’ Ustaarabu ulikuwepo kwa kiasi kikubwa, na hata ikafika mahali mtu unajisahau kwamba umepanga. Unajihisi kwamba umejenga!
Kizungumkuti kilianza pale kampuni yetu ilipogundua kwamba nyumba ni rasilimali inayoweza kuingiza mapesa tele, mbali na miradi ya kampuni. Amri ikatoka wote tuhame.
“Hii ni kuwawezesha mume na wazo la kujijengea nyumba zetu wenyewe!” walidai.
Pamoja na upinzani geresha uliotolewa na chama kisichosajiliwa, cha kutetea wafanyakazi, hatimaye wote tuliziacha nyumba za kampuni.
Mimi nilihamia kwenye nyumba ya kupanga kule uswahilini.
Na kwa kuwa nilikuwa `bachela,’ nilipanga chumba kimoja, hasa pia kutokana na ukweli kwamba kuishi kwenye nyumba ya kampuni kulinifanya nisiwe na vyombo vingi vya ndani. Kila kitu nilikikuta kwenye nyumba ya kampuni.
Kutokana na kazi zangu ni mtu ninayetoka asubuhi sana na kurudi usiku. Hivyo sikuwa na muda wa kujua yanayoendelea nyumbani pale.
Lakini kadiri muda ulivyoenda ndivyo nilivyoanza kusikia maneno maneno ya umbe na udaku kutoka kwa wapangaji wenzangu.
“Anaringa sana bwana yule! Anajifanya yeye ndiyo yeye!” walidai.
Nikawapuuza.
Niliamini kwamba chura hawezi kumzuia binadamu kuteka maji kwenye kisima chake. Ataishia kupiga mayowe ya bure tu.
Maneno yaliendelea, hata hivyo.
Mwishowe yakaingia kuwa ni majungu.
“Mtu huyu anatudharau sana! Anaingia anajiona eti ana pesa! Angekuwa nazo si angejenga!” alisema mmoja wao kwenye kikao chao cha umbea kwenye korido.
“He, He, Heee! Halooo!” walicheka kwa pamoja.
“Haikufaa nazi, itaweza koroma?”
Kwa kuwa sikumdharau mtu, niliona ni upuuzi tu maneno yao. Kumbe nao waligundua sijali mambo yao. Wakaenda kutia fitna kwa mwenye nyumba.
Niliondolewa kwa maelezo kwamba “wakwe wamekuja” hivyo `baba mwenye nyumba’ hana pahala pengine pa kuwaweka.
Sheria za nyumba ziko mahakaman tu. Huku uswahilini hazipo. Mwenye nyumba ndiye mfalme.
Nilihama.
Kwenye nyumba hii niliyohamia, `baba mwenye nyumba’ tulikuwa naye pale pale. Hii ikaongeza mitafaruku zaidi. Alipenda kuingilia maisha yetu ya kila siku.
Alituzuia kuleta wageni pale nyumbani kwa sababu `watajaza choo’. Nilikuwa kizungumkuti siku ile Wafanyakazi wenzangu walipokuja kunipa pole ya kuumwa.
“Unaleta kampuni nzima nyumbani!” alifoka. “Wanajaza choo tu!” Nilijihisi aibu na kudhalilishwa. Lakini mfanyakazi mwenzetu, Bennie yeye `fyatu’ huwa hakopeshi.
“Ah mzee maneno gani hayo!” Kibanda hiki kukijenga unaona umefika? Watu tumeona nyumba itakuwa kibanda hiki?”
Alichokoza nyuki. Yalifuata mabishano makali na kurushiana maneno. Na kama unavyojua, uswahilini hamna dogo. Yalikuja makundi ya watu kutafuta umbea wa kueneza mtaani.
Tangu siku hiyo Mzee Nguri, mwenye nyumba, alinipigia mahesabu ya kunitimua. Alifanya vitimbi na vitimvi, mpaka mwenyewe nikainua mikono.
Kodi yangu ya miezi sita ilipoisha tu, nikahamia nyumba nyingine ya kupanga. Huku huku uswahilini.
Mwenye nyumba niliyohamia naye alikuwa akiishi humo humo. Hii ilikuwa na masharti hatari tupu!
Mbali na masharti `ya kawaida’ ya nyumba za kupanga, kwenye nyumba hii mambo yalizidi.
Kwanza haikuruhusiwa kupiga mluzi nyumbani mle. Lilikuwa ni kosa `la jinai’ kuthubutu kuchonga ulimi na kupiga mluzi.
Haikuruhusiwa kabisa kuingia chooni pasipo kukohoa kidogo, wakati wa kuingia na wakati wa kutoka.
Wakati wa maakuli, ilikuwa ni lazima kuangusha sakafuni tonge la kwanza.
Kupika nyama ya nguruwe, ndani ya nyumba ile ilikuwa ni marufuku na makufuru kabisa!
Sikuwa na ujanja.
Ilibidi kukubali masharti yote hayo, na mengine ya ajabu ajabu.
Zilipita siku na siku za uvumilivu. Kukubali masharti yale kulitaka moyo, na moyo wenyewe mkubwa. Lakini kwa mtu ambaye hakuwahi kwenda hata kwa mganga wa kienyeji, masharti yale yalikuwa komesha.
Abdillahi, mwenye chumba jirani na mimi, siku moja aliacha kudondosha tonge kama `amri ya tatu’ ya `baba’ mwenye nyumba inavyosema.
“We Abdilahi, unafanya nini?” alifoka mzee Fyumi, baba mwenye nyumba,” kwa nini hukutupa tonge la kwanza? Haya tupa ugali wote upesi!”
Abdilahi alitaka kujikojolea. Chumba kimefungwa, mzee Fyumi amejuaje?”
Aliutupa ugali huo sakafuni.
Alikaa anatetemeka. “Kwa hiyo mzee Fyumi anaona kila kitu chumbani humu!”
Walipokuwa wakijibizana na mzee Fyumi, kila mtu alisikia.
Na kila mtu alistaajabu.
Nikaanza kufikiria mara mbili namna ya kujikwamua. Ni wakati huo nilipopata kiwanja pale bondeni. Siyo kwamba sielewi madhara na maradhi ya kukaa bondeni, katu! Nilitaka kukwepa matatizo ya nyumba za kupanga. Viwanja vya sehemu nyingine bei yake mtu huwezi kujikusuru na kununua.
Kazi ikawa kwenye kujenga. Sikuwa hata na thumni! Ilibidi kufunga mikanda.
Hapo ujue maisha ya pale nyumbani hayakuwa na raha, hasa kwa vile nikikumbuka tafrani zilizomkubwa Abdilahi. Nilianza kupiga mahesabu ya jinsi ya kujenga japo ka-chumba kamoja, ndio nihamie.
Siku moja niliinia chooni bila kukohoa. “Mambo haya maanake nini?” nilisema.
Wakati nafunga mlango wa chooni tu, nikaanza kudundwa mangumi na mtu nisiyemwona.
“Mama wee! nakufaa!” nilipiga mayowe.
Yule mtu nisiyemwona aliendelea kunitwanga mingumi pasi na huruma. Uzito wa ngumi zake Tyson haoni ndani. Ngumi zilinichanganya mpaka nikashindwa kuona mlango.
“Nakufa mama wee!”
Watu wakajaa nje ya choo. Niliweza kuwasikia wengine wakipia makelele. Lakini kelele zao hazikumzuia yule aliyenigeuza mfuko wa kufanyia mazoezi ya ndondi.
Damu zilianza kunitoka puani. Kizunguzungu kikaanza kunishika. Hata sauti yangu ikaanza kufifia. Ndipo kwa mbaali nikamsikia mzee Fyumi.
“Pumbafu! Unajidai kuleta usomi wako uchwara hapa!” alifoka baba mwenye nyumba, kule kule nje. Nilidhani atanionea huruma aingie aje anisaidie lakini hakuja.
“Hebu chukua ndala yako ya kushoto ujipige nayo kisogoni!”
Nilichukua kandambili na kujipiga nayo kisogoni, huku ngumi za nguvu zikiniaga.
Hata haja niliyoenda nayo chooni ilipotea. Nilirudi chumbani huku kundi la watu likinikodolea macho. Majeraha niliyokuwa nayo nisingeweza kutibiwa bila PF3.
Nilijua polisi wasingeelewa hadithi hii ya kupigwa na mtu asiyeonekana. Nilidai nimepigwa na vibaka!
Kazini nilipewa `ofu’ ya wiki nzima nikijiganga majeraha.
Hakikubaki kitu kingine zaidi ya kuhama. Lakini kuhama vivi hivi pasi na kulipiza kisasi sikuona ni vema.
Tukaandaa mkakati. Miye ndiye kinara wa mkakati ule.
“Lazima tumkomeshe!” nilisema.
Tulijua ratiba za mzee Fyumi. Kila Jumamosi hutoka na kwenda mahali anakokujua mwenyewe. Hurudi jioni, wakati wa jua kupunga.
Siku ile sint’oisahau. Siku ya kutekeleza mkakati wetu.
Siku hiyo kila mtu alipika `mkuu wa meza’ kwenye chumba chake, kinyume na amri ya mzee Fyumi. Na badala yaa kudondosha tonge la mwanzo, tuliangusha vipande vya vyama ya nguruwe.
Tulifanya uchokozi mkubwa.
Na tulijua pia kuwa tumetangaza vita. Ila hatukuwa na uhakika nani mitutu itamuelekea.
Hakikutokea kitu.
Lakini hamna aliyeondoka nyumbani. Kila mmoja alingoja kuona hatma ya `maskadi’ tuliyoyatega. Sijui `mibomu’ hii itatulipukia wenyewe kama mzee wa Kiraracha? Au mibomu hiyo itapita tageti?!
Na kweli. Hofu yetu haikuwa ya bure.
Jioni ile mzee Fyumi alirudi. Ile anakanyaga tu kizingiti cha mlango wa nyumba yake, alianza kupata kipigo cha nguvu kuliko nilichokipata miye.
“Nakufaa mwee!” alipiga mayowe. Lakini kipigo kikaendelea.
Nikahisi kiasi kidogo cha huruma kikiteleza moyoni mwangu.
“Maskini mzee Fyumi!” nilisema.
Alitimua mbio kuelekea anakokujua. Jioni ile walikuja ndugu zake na kututimua kwa notisi ya masaa.
Nilihamia kwenye kibanda changu kisichokamilika. Potelea mbali! Afadhali hivi kuliko mateso ya nyumba za kupanga.
Kero za mafuriko ni za msimu, kero za nyumba za kupanga ni za mwaka mzima. Hivi siwaelewi kabisa wale wote wanaodai nihame bondeni. Wengine wanadhani `nimelogwa’ ndiyo maana sihami.
Wangejua!










NYAKACH KILLINGS!
BETHANY CHILDREN'S HOME TANZANIA




